IQNA

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei

Iran haitaafiki mjadala kuhusu uwezo wake wa kiulinzi

20:41 - October 25, 2017
Habari ID: 3471230
TEHRAN (IQNA)-Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uwezo na nguvu za kiulinzi za Iran si kitu cha kujadiliwa kabisa kama ambavyo zana zozote za ulinzi na kitu chochote kile kinacholeta nguvu za taifa la Iran si kitu cha kufanyiwa muamala wa aina yoyote ile.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo leo katika sherehe za pamoja za kuhitimu masomo, kula viapo na kupandishwa daraja wanachuo wa Chuo Kikuu cha Maafisa wa Kijeshi cha Imam Ali AS na kubainisha kwamba: Maadui wa Jamhuri ya Kiislamu wanaumizwa na mambo yanayolipa nguvu taifa la Iran na ndio maana wanapinga sana kuongezeka nguvu za Jamhuri ya Kiislamu kati ya mataifa ya dunia, ya eneo hili na nje ya eneo hili.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameutaja upinzani unaooneshwa na madola ya kibeberu dhidi ya uwezo wa kiulinzi wa Iran kuwa unatokana na woga wao na kusisitiza kwamba, njia ya kukabiliana na upinzani wao huo ni kufanya kinyume na wanavyotaka mabeberu hao, yaani kujiimarisha kiulinzi na kitaifa na kusimama imara kukabiliana na njama zao.

Ayatullah Khamenei aidha amesema jukumu kubwa la maafisa wa vikosi vya ulinzi vya Iran ni kuimarisha usalama wa nchi na kusisitiza kuwa: Maendeleo yote; yawe ya kielimu, kiviwanda na kiuchumi yanahitajia kuwepo usalama nchini.

Amirijeshi Mkuu wa vikosi vyote vya ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekumbusha kuwa, kuna wakati na licha ya Iran azizi kuwa na historia kongwe inayong'ara na yenye watu wenye vipaji visivyo na kifani, lakini ilikuwa dhaifu, ilidhalilishwa na iliingia mikononi mwa viongozi tegemezi kiasi kwamba ilikuwa inategemea ushauri kutoka kwa Wamarekani, Wazayuni na Uingereza, lakini Uislamu umeiokoa Iran na kulitunuku taifa hili Jamhuri ya Kiislamu ambayo imeifanya Iran kuwa yenye nguvu na heshima kubwa.

3656695

captcha