IQNA

Idul Fitr

Ayatullah Khamenei aongoza Sala ya Idul-Fitr mjini Tehran

IQNA - Makumi ya maelfu ya waumini leo Jumatano asubuhi walikusanyika kwenye Uwanja  wa Swala wa Mosalla Imam Khomeini katika mji mkuu wa Iran, Tehran, kwa ajili ya  Sala ya Idul Fitr inayoashiria kumalizika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Sala hiyo iliongozwa na Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Sala hiyo ilihudhuriwa na maafisa wakuu wa mihimili ya dola nchini Iran pamoja na makamanda wa kijeshi,wananchi wa matabaka mbali mbali na wanadiplomasia wa kigeni.

Sala ilisaliwa saa mbili unusu asubuhi, lakini umati wa watu ulianza kufika katika uwanja huo mkubwa wa Swala mapema Alfajiri.

Mapema Siku ya Jumanne, Iran ilitangaza kwamba baada ya kuonekana kwa mwezi, Jumatano itakuwa sikukuu ya Idul Fitr. Hii ni siku  ambayo huadhimisha mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, ambao huwa na siku 29 au 30.

Katika nchi nyingi za Kiislamu na hata zisizo na Kiislamu, ikiwa ni pamoja na Iran, kamati za kutazama mwezi huundwa ili kuthibitisha kuanza kwa mwezi wa Shawwal.

4209700