Ayatullah Seyed Ahmad Khatami, khatibu wa Sala ya Ijumaa mjini Tehran amelaani jinai ya kigaidi siku ya Jumatano katika maziara ya mashahidi wa mji wa Kerman huko kusini mashariki mwa Iran. Aidha ameashiria mauaji ya raia 17,000 wa Iran katika hujuma za kigaidi baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kusema: Kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) liliundwa na Marekani na ni chombo cha utawala wa Kizayuni wa Israel.
Ikumbukwe kuwa katika hotuba ya kampeni ya Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump mwaka 2016, alimtuhumu mtangulizi wake Barack Obama, kuwa ndiye aliyeanzisha kundi la kigaidi la Daesh.
Ayatullah Khatami amesema kuwa, kundi la kigaidi la Daesh lina hasira kwa sababu liliangamizwa Iraq na Syria kufuatia jitihada za Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyeuawa shahidi, na akasisitiza kwamba damu ya mashahidi wa tukio la kigaidi la Kerman italipizwa kisasi.
Shambulio la kigaidi lililotekelezwa juzi Jumatano huko Kerman limeua shahidi watu wasiopungua 89 na kujeruhi wengine 285. Hujuma hiyo ya kigaidi ilitekelezwa katika kumbukumbu ya kumuenzi Kamanda wa vita dhidi ya ugaidi Shahidi Luteni Jenerali Qassim Soleimani aliyeuliwa kigaidi katika hujuma ya jeshi katili la Marekani huko Baghdad Iraq miaka minne iliyopita. Kundi la kigaidi la Daesh limedai kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi nchini Iran.
4192130