IQNA

Hali Saudia

Saudia yakosolewa kwa kuwafunga jela wahubiri wanaopinga utawala wa kifalme

14:18 - September 15, 2022
Habari ID: 3475785
TEHRAN (IQNA)- Jumuiya 16 za Kiislamu duniani zimetoa tamko la kulaani hukumu kali za vifungo jela dhidi ya walinganiaji wa Kiislamu wa Saudi Arabia zilizotolewa hivi karibuni na mamlaka ya mahakama ya Saudia.

Ukandamizaji wa uhuru wa kujieleza na ukiukwaji wa haki za binadamu nchini Saudi Arabia si suala geni na lina mizizi katika historia ya utawala wa ukoo wa Al Saud, lakini suala hilo limeshadidi zaidi katika kipindi cha hivi karibuni, hasa katika ufalme wa Salman bin Abdulaziz na mrithi wa taji la ufalme, Muhammad bin Salman, kutokana na matendo ya kuaandama na kuwafutilia mbali wapinzani.

Katika wiki zilizopita, mfumo wa mahakama wa Saudia ulitoa hukumu ya vifungo vya muda mrefu jela kwa wahubiri kadhaa wa Kiislamu na kuongeza adhabu ya Sheikh Nasser al-Omar kutoka miaka 10 hadi 30. Vilevile Sheikh Abdul Rahman Al-Mahmoud amehukumiwa kifungo cha miaka 25, Sheikh Essam Al-Owaid miaka 27 na Sheikh Ibrahim Al-Dawish miaka 15 jela.

Taarifa ya pamoja ya jumuiya za Kiislamu duniani kote imesema, kutolewa kwa hukumu za muda mrefu jela dhidi ya wanazuoni na wahubiri wa Kiislamu wa Saudia kunaweza kuwa utangulizi wa kutolewa hukumu za kifo dhidi ya "Salman al-Ouda", "Awad bin Mohammed Al-Qarni" , "Ali Al-Omari" na wahubiri wengine wa Kiislamu wa Saudia.

Taarifa hiyo ya pamoja ya jumuiya 16 za Kiislamu duniani imesema, badala ya kuwaheshimu wasomi na wahubiri wa kidini ambao wengi wao ni wazee, Saudi Arabia inawafunga na kuwatesa.

Jumuiya hizo za Kiislamu zimesisitiza kwamba hukumu hizo za kidhalimu zimetolewa kwa kuzingatia uongo, dhana zisizo na mashiko, na vinyongo vya mfumo wa mahakama wa Saudia.

4085537

captcha