IQNA

Sayyid Hassan Nasrallah

Nasrallah alaani hujuma ya kigaidi Niece Ufaransa na pia matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu ya Macron

14:19 - October 31, 2020
Habari ID: 3473313
TEHRAN (IQNA) Kiongozi wa Harakati ya Hizbullah ya Lebanon amelaani hujuma ya hivi karibuni ya kigaidi Ufaransa na wakati huo huo pia amelaani matamshi ya chuki dhidi ya Uislamu ya Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo.

Televisheni ya Al Manar imemnuku Sayyid Hassan Nasrullah Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon akisema hayo usiku wa kuamkia leo Jumamosi katika hotuba muhimu aliyoitoa kwa mnasaba maadhimisho ya Maulid ya Bwana Mtume Muhammad SAW na sambamba na kulaani shambulizi la Alkhamisi usiku lililotokea katika mji wa Nice huko Ufaransa amesema, makundi ya Kiislamu yanalaani kitendo hicho na vingine mfano wake iwe vya hivi sasa au vya huko nyuma na hayakubaliani kabisa na mashambulizi kama hayo.

Sayyid Hassan Nasrallah amesema kuwa, jinai zinazofanywa na magenge ya kigaidi yaliyoundwa na kuungwa mkono na madola ya Magharibi, hazina uhusiano wowote na Mtume Muhammad SAW wala umma wa Kiislamu na amezitaka nchi za Magharibi ziache kuyalinda magenge hayo ya ukufurishaji.

Aidha amesema, viongozi wa Ufaransa hawana ruhusa ya kuhusisha kitendo cha mtu mmoja na mafundisho matukufu ya Uislamu na kusisitiza kuwa, kama itatokezea Mkristo fulani amefanya uhalifu, si sahihi kwetu kuwahusisha Wakristo wote na uhalifu wa mtu huyo. Sayyid Nasrallah amemkosoa vikali rais wa Ufaransa, Emmaneul Macron kwa matamshi yake ya hivi karibuni na kusema, rais huyo hakupaswa kabisa kudai kuna ugaidi na ufashisti wa Kiislamu.

Amesema, hakuna Muislamu yeyote anayehusisha na Ukristo, jinai za Marekani na nchi za Ulaya katika pembe mbalimbali za dunia kama vile Algeria, Libya na Afghanistan, wala humsikii Muislamu yeyote akisema kuna ugaidi na ufashisti wa Kikristo kutokana na jinai hizo kubwa zinazofanywa na nchi hizo za Wakristo. 

Aidha amesema, wanachopaswa viongozi wa Ufaransa ni kujibu swali la kwamba kwa nini kutilia shaka tu ngano ya Holocaust ya kuuliwa Mayahudi na Wanazi wa Ujerumani ni kosa kubwa kwa mtazamo wa viongozi wa Magharibi, lakini kumtukana na kumvunjia heshima Bwana Mtume Muhammad SAW, rehema ya walimwengu wote ni uhuru wa kusema? Vipi jambo hilo linaingia akilini?

Nasrallah amewataka wakuu wa Ufaransa waache kuulaumu Uislamu na Waislamu kutokana na vitendo vya kigaidi na kwamba wanaotenda vitendo hivyo viovu wanapaswa kuadhibiwa kama wahalifu. Halikadhalika amewataka wakuu wa Ufaransa wafahamu kuwa, Waislamu katu hawawezi kukubali kuona Mtume Muhammad SAW akidhalilishwa.

3932141

captcha