IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Iran haitafanya mazungumzo na Marekani, mashinikizo yamefeli

13:53 - September 17, 2019
Habari ID: 3472134
TEHRAN (IQNA) - Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria kauli mpya zilizotolewa na Marekani kuhusu mazungumzo na akasisitiza kwamba: Viongozi wote wa Jamhuri ya Kiislamu wanakubalina kwa kauli moja kuwa, hayatafanywa mazungumzo na Marekani katika ngazi yoyote ile.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei ameyasema hayo mapema leo Jumanne mjini Tehran wakati wa ufunguzi wa darsa yake ya  marhala ya juu kabisa ya Fiqhi (Bahthul Kharij) sambamba na kuanza mwaka mpya wa masomo katika vyuo vikuu vya kidini hapa nchini vya Hawza.

Amesema, lengo la Marekani la kutumia mbinu ya mazungumzo ni kutaka kutwisha matakwa yake na kuthibitisha kuwa mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa yamekuwa na taathira kwa Iran. Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa, sera za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa katika kukabiliana na taifa la Iran hazina maana wala thamani yoyote.

Ayatullah Khamenei ameashiria misimamo tofauti ya viongozi wa Marekani kuhusu mazungumzo na akasema: Baadhi ya wakati wanasema, ni mazungumzo bila masharti yoyote, na wakati mwingine wanasema, mazungumzo kwa kutekeleza kwanza masharti 12. Kauli kama hizi ama zinatokana na siasa zao za kuchanganyikiwa au ni mbinu ya kuukanganya upande wa pili. Lakini bila shaka Jamhuri ya Kiislamu haitababaika, kwa sababu njia tunayofuata iko wazi kabisa na tunajua tunachokifanya.

Amesisitiza kuwa: Kwa ajili ya kufanya mazungumzo ya aina hii inapasa wawaendee watu ambao, wanayowafanyia ni mithili ya ng'ombe wa kukamwa maziwa; lakini Jamhuri ya Kiislamu ni jamhuri ya waumini, jamhuri ya waliojisalimisha kwa Allah na jamhuri ya izza na heshima.

Kiongozi Muadhamu ameeleza bayana kwamba: Ikiwa Marekani itaachana na kauli zake hizo na kutubia, na ikarejea kwenye makubaliano ya nyuklia iliyoyakiuka, wakati huo ndipo nayo pia itaweza kushirki kwenye mazungumzo ya pamoja na nchi zingine shiriki kwenye makubaliano hayo, zinazofanya mazungumzo na Iran; kinyume na hivyo hakuna mazungumzo yatakayofanywa katika ngazi yoyote baina ya viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu na Wamarekani, si New York, si pengine popote pale.

Ikumbukwe kuwa, baada ya hatua ya upande mmoja na ya kuhalifu sheria iliyochukuliwa na Marekani mnamo mwezi Mei 2018 ya kujitoa katika makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA, Iran ilitekeleza kwa muda wa mwaka mzima kile ilichokiita "subira ya kistratejia" na kutoa muhula kwa pande zingine hususan nchi za Ulaya kutekeleza ahadi zao za kufidia kujitoa Marekani kwenye makubaliano hayo.

Kutokana na kushindwa kufanya hivyo, kuanzia Mei 8 mwaka huu, Iran ilianza kupunguza uwajibikaji wake katika JCPOA kulingana na vifungu vya 26 na 36 vya makubaliano hayo.

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Ayatullah Khamenei amesema katika kipindi cha miaka 40 tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikikabiliana na kila aina ya njama lakini maadui hawajaweza kuisambaratisha Iran. Amebainisha kuwa ni sera za hao maadui ambazo zimekuwa zikisambaratisha na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuongeza  kuongeza kuwa: "Katika mustakabali pia, kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu, Iran itaendelea kusambaratisha maadui na kuibuka mshindi katika medani."

3842725

captcha