IQNA

Meya Mwislamu New Jersey Marekani asailiwa masaa matatu kuhusu ugaidi

11:30 - September 14, 2019
Habari ID: 3472129
TEHRAN (IQNA) – Meya Mwislamu huko New Jersey nchini Marekani amesema alishikiliwa kwa muda katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa John F. Kennedy mjini New York mwezi uliopita ambapo maafisa wa usalama walimsaili kuhusu iwapo anawafahamu magaidi.

Meya wa eneo la Prospect Park katika jimbo la New Jersey Mohamed Khairullah anasema alishikiliwa katika uwanja huo wa ndege kwa muda wa masaa watatu mwezi Agosti na kusailiwa na maafisa wa usalama wa Idara ya Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani (CPB).

Khairullah alisiamishwa na maafisa hao wa Usalama akiwa ameandamana na mke wake na watoto wake wanne wakitokea Uturuki kutembelea jamaa zao.

"Bila shaka kitendo hicho kiliniumiza sana na nilitafakari na kusema hii si Marekani ambayo naifahamu," amesema Khairullah ambaye amekuwa meya wa Prospect Park tokea mwaka 2006. Ameongeza kuwa: "Mimi ninazifahamu vizuri sheria na katiba yetu,  na hivyo kila kitu nilichofanyiwa hapo (katika uwanja wa ndege) ni kinyume cha sheria."

Wakili mkuu wa  Baraza la Mahusiano ya Kiislamu nchini Marekani (CAIR), Ahmed Mohamed amesema maafisa wa usalama walimuuliza Khairullah masuala kadhaa kuhusu kazi yake, majina ya mama yake, safari yake Uturuki na iwapo alikutana wakuu wa makundi ya kigaidi akiwa huko.

Mohamed amesema ni wazi kuwa Khairullah alisimamishwa na kusailiwa kwa sababu tu yeye ni Mwislamu na kuongeza kuwa idadi kuwa ya wasafiri Waislamu nchini Marekani wamekuwa wakiakbiliwa na ubaguzi huo kwa muda wa miaka mingi sasa. Aidha Khairullah amesema simu yake ya mkononi ilichukuliwa na maafisa wa usalama na wakakaa nayo kwa muda wa siku 12 jambo ambalo amesema yamkini ni ukiukaji wa katiba.

Wakili mkuu wa CAIR amesema Khairullah atapambana kuhakikisha kuwa haki za Wamarekani wengine hazikiukwi.

CAIR inasema uchunguzi umebaini kuwa, hatua ya utawala wa Rais Donald Trump kupiga marufuku Waislamu kutoka baadhi ya nchi kuingia nchini humo ni jambo ambalo limechangia kuongezeka chuki dhidi ya Uislamu nchini humo.

Ripoti ya CAIR iliyochapishwa mwaka jana chini ya anuani ya "Waliolengwa" ilibaini kuwa utawala wa Trump unawalenga kwa makusudi Waislamu raia wa Marekani, amesema Mkurugenzi Mkuu wa CAIR Nihad Awad.  CAIR inasema uchunguzi wake umebaini kuongezeka chuki lisilo na kifani la chuki dhidi ya Waislamu na watu wa jamii nyinginezo za wachahce nchini humo tokea Trump aingie madarakani Januari 2017.

3469388/

captcha