IQNA

Waislamu wa Madhehebu ya Shia waadhimisha Sikukuu ya Ghadir

12:40 - August 20, 2019
Habari ID: 3472092
TEHRAN (IQNA)- Waislamu wa madhehebu ya Shia kote duniani leo wanaadhimisha sikukuu ya Ghadir ambayo ni kati ya siku muhimu zaidi katika kalenda ya historia ya Uislamu.

Leo ni Jumanne tarehe 18 Dhulhija 1440 Hijria inasadifiana na 20 Agosti mwaka 2019. Siku kama hii ya leo miaka 1430 iliyopita Mtume Muhammad SAW akiwa katika safari yake ya mwisho ya Hija, kwa amri ya Mwenyezi Mungu alimtangaza Imam Ali bin Abi Twalib AS kuwa kiongozi wa Waislamu wote baada yake.
Hatua hiyo ya Mtume Mtukufu ilifanyika katika eneo linalojulikana kwa jina la Ghadir Khum katika makutano ya njia ya Makka na Madina. Siku hiyo Mtume SAW alitoa hotuba mbele ya hadhara kubwa ya Waislamu kisha akashika mkono wa Ali bin Abi Twalib na kusema: "Kila mtu ambaye mimi ni kiongozi wake basi huyu Ali pia ni kiongozi wake. Mwenyezi Mungu ampende atakayempenda, na amfanyie uadui atakayemfanyia uadui."
Mtume SAW pia aliwausia Waislamu kushikamana na Qur'ani na Ahlubaiti wake na akasema viwili hivyo havitatengana hadi vitakapomkuta yeye katika Hodhi ya Kauthar, Siku ya Kiyama.
Baada ya maneno hayo ya Mtume, malaika wa wahyi aliteremka kwa Mtume na kumsomea aya ya 3 ya Suratul Maidah ambayo inasema: "Leo nimekukamilishieni dini yenu, na kukutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni Uislamu uwe dini yenu."
Tukio muhimu la Ghadir Khum limechunguzwa na kuzungumziwa na wasomi wengi wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu. Abul Faraj bin Jauzi Hambali, mmoja wa wanafikra na wasomi wa Kiislamu wa madhehebu ya Kisuni ya Imam Hambali anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: "Wataalamu wa historia na sira ya Mtume, wote wanaafikiana kwamba, tukio la Ghadir lilitokea wakati Mtume (SAW) alipokuwa njiani kurejea Madina katika Hija yake ya mwisho. Katika siku hiyo masahaba, Waarabu na wakazi wa viunga vya mji wa Makka wapatao laki moja na elfu 20 walikuwa na Mtume. Hiyo ndiyo idadi ya watu walilosikia hadithi inayohusiana na uongozi wa Ali (AS) kutoka kwa Mtume katika siku ya Ghadir."
Maulamaa wengine wengi wa Kisuni kama Tirmidhi, Ibnu Majah, Ibn Asaakir, Ibn Naiim, Ibn Athir, Khorazmi, Suyuti, Ibn Hajar, Haithami, Ghazali pamoja na Bukhari wamelitaja tukio la Ghadir katika vitabu vyao. Abu Sa'ad Mas'uud bin Nasir Sajistani, mmoja wa maulamaa wa Kisuni ameeleza katika kitabu chake kiitwacho Ad Dirayah fii Hadithil Wilayah kuwa ameinukuu hadithi hii kutoka kwa masahaba 120 wa Bwana Mtume.

3469207/

captcha