IQNA

Taarifa ya IRGC

Iran ilisimamisha meli mafuta ya Uingereza kwa kuvunja sheria za kimataifa

22:24 - July 20, 2019
Habari ID: 3472049
TEHRAN (IQNA) - Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran IRGC limetangaza kuwa limesimamisha meli moja ya mafuta ya Uingereza baada ya kukiuka sheria za kimataifa za ubaharia katika Lango Bahari la Hormuz.

Taarifa ya Idara ya Uhusiano Mwema ya IRGC imeeleza bayana kuwa, hatua hiyo ya kuzuia meli ya mafuta ya Uingereza kwa jina la "Stena Impero” imetekelezwa kikamilifu katika fremu ya sheria za ndani ya nchi na vilevile za kimataifa kuhusiana na masuala ya safari za baharini.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, meli hiyo ilisimamishwa Ijumaa na jeshi la IRGC kufuatia ombi la Mamlaka ya Bandari ya Hormozgan na vilevile Shirika la Ubaharia, baada ya chombo hicho kuvunja sheria kadhaa za safari za baharini.
Shirika la Northern Marine linalomiliki meli hiyo yenye bendera ya Uingereza limesema meli hiyo ya mafuta ilikuwa na mabaharia 23. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekanusha vikali madai ya kipropaganda ya vyombo vya habari vya Magharibi kwamba Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran limezuia meli ya pili ya mafuta ya Uingereza katika Ghuba ya Uajemi.
Jeremy Hunt, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza amedai kuwa Iran itaandamwa na adhabu kali kwa kuzuialia meli mbili za Uingereza iwapo kadhia hiyo haitafumbuliwa haraka iwezekanavyo.
Siku ya Alhamisi pia Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, baada ya kuhakikisha kwamba meli moja ya kigeni ilikuwa imebeba lita milioni moja za mafuta ya magendo, na kupata kibali kutoka kwa maafisa husika wa vyombo vya mahakama vya humu nchini, lililazimika kuisimamisha meli hiyo kusini mwa Kisiwa cha Larak katika Ghuba ya Uajemi.
Eneo la Ghuba ya Uajemi na hasa Lango Bahari la Hormoz, lina nafasi muhimu katika uchumi wa dunia, hivyo jukumu la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika kulinda usalama wa eneo hilo lina umuhimu wa kistratijia.
Katika uwanja huo, Hussein Salami, Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu alisema jana kwamba eneo la Ghuba ya Uajemi, Lango Bahari la Hormoz na visiwa vinavyolizunguka ni eneo nyeti, muhimu na lisilotenganishika na uchumi wa dunia, si kwa Iran pekee, bali kwa ulimwengu mzima.

3828610

captcha