IQNA

Maulamaa wa Kiislamu walaani wakuu wa nchi za Kiarabu waliokutana na Netanyahu

10:45 - February 19, 2019
Habari ID: 3471846
TEHRAN (IQNA)- Jumuiya ya Kimataifa ya Maulama wa Kiislamu imelaani vikali mkutano wa hivi karibuni baina ya maafisa wa ngazi za juu wa nchi za Kiarabu na Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni wa Israel huko Warsaw, Poland.

Jumuiya hiyo ilituma taarifa kupitia Twitter Jumapili na kusema: " Jumuiya ya Kimataifa ya Maulama wa Kiislamu imesikitishwa na mkutano wa baadhi ya maafisa wa nchi za Kiarabu na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu. Utawala wa Israel unakalia kwa mabavu ardhi takatifu za Kiislamu, unaua watoto Wapalestina, unaweka mzingiro katika miji ya Palestina na unatekeleza sera za Kuyahudisha Palestina na hasa Quds Tukufu (Jerusalem) kwa msaada wa Marekani."

Wakati huo huo Spika wa Bunge la Kuwait amekosoa vikali ushiriki wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Nchi hiyo katika mkutano wa Warsaw, Poland ambao ulihudhuriwa pia na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Utawala Haramu wa Israel.

Sambamba kuendelea upinzani mkubwa wa hatua ya baadhi ya viongozi wa nchi za Kiarabu ya kuboresha mahusiano na utawala haramu wa Kizayuni, Marzouq Al-Ghanim, Spika wa Bunge la Kuwait amesema kuwa katika kujadili masuala ya kiasa na matokeo ya kikao cha Warsaw, atamwita Sabah Al-Khalid Al-Sabah, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo kujieleza bungeni.

Siku ya Jumapili pia, Makumi ya maelefu ya watu wa Yemen wameanadamana kote katika nchi hiyo kulaani nchi za Kiarabu ambazo zinatekeleza usaliti kwa kuanzisha mchakato wa kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel. Maandamano hayo yamefanyika katika mji mkuu Sana'a na pia katika mikoa ya magharibi mwa nchi hiyo ya Sa’ada, al-Hudeydah, Ta’izz, na al-Jawf kati ya maeneo mengine.

Awali Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina alikuwa ametoa mwito kwa nchi za Kiarabu kususia mkutano wa Poland, ulioitishwa na kufadhiliwa na Marekani.

Riadh al-Maliki alisema  kuwa, iwapo Waarabu lazima washiriki mkutano huo, kwa uchache wanapaswa kutuma maafisa wa ngazi za chini. Hatahivyo wakuu wa nchi za Kiarabu walipuuza wito huo na walishiriki katika vikao vya siri na Netanyahu.

Mkutano wa Warsaw, mji mkuu wa Poland ulioitishwa na Marekani na washirika wake, ulifanyika kati ya tarehe 13 na 14 ya mwezi huu kwa lengo la kujadili kile kilichotajwa kuwa ni 'Usalama wa eneo la Mashariki ya Kati.' Hatahivyo ajenda kuu ya mkutano huo lilikuwa ni kushawishi kuwekwa kando na kupuuzwa kadhia ya Palestina katika uga wa kimataifa na kuchochea chuki dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

3467953

captcha