IQNA

Fainali za Mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Iran kuanza Aprili 10

11:00 - February 05, 2019
Habari ID: 3471831
TEHRAN (IQNA)-Fainali za Mashindano ya 36 ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu zimepangwa kuanza mjini Tehran kuanzia Aprili 10.

Akizungumza na mwandishi wa IQNA, Mkuu wa Taasisi ya Mashindano ya Qur'ani katika Shirika la Wakfu la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hujjatul Islam Ali Moqanni amesema fainali za mashindano hayo zitafanyika katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini.

Aidha amesema kutakuwa na mabadiliko katika mashindano ya mwaka huu ikilinganishwa na mashindano yaliyopita.

Kwa mfano, mwaka huu kutakuwa na raundi tatu, ambapo katika raundi ya kwanza washiriki watatuma fomu za maombi ya kushiriki zikiwa zimeambatana na faili la sauti ya qiraa yao. Amesema wale watakaoonekana wana viwango vinavyostahiki, wataalikwa Iran kushiriki katika mashindano ya nusu fainali ambayo yatafanyika Aprili 9.

Hatimaye fainali zaitaanza tarehe 10 Aprili katika Ukumbi wa Sala wa Imam Khomeini. Hujjatul Islam Moqanni amesema mashindano yatamalizika kwa washindi kutunukiwa zawadi Aprili 14 na hatimaye washiriki wote watakutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu mnamo Aprili 15.

Sawa na miaka iliyopita, mashindano ya mwaka huu pia yatakuwa na vitengo maalumu vya mashindano ya wanawake, wanafunzo wa vyuo vya kidini na wanafunzi wa shule.

Shirika la Wakfu la Iran huandaa mashindano ya kimatiafa ya kusoma na kuhifadhi Qur'ani ya Iran kila mwaka ambapo huwa na washiriki kutoka kila kona ya dunia.

Mwaka jana kulikuwa na washiriki 370 wa kigeni waliohudhuria mashindano ya kimataifa ya Qur'ani.

3786715/

captcha