IQNA

CNN yamtimua mchambuzi wake ambaye ameunga mkono haki za Wapalestina

11:31 - December 01, 2018
Habari ID: 3471757
TEHRAN (IQNA) Kanali yaTelevisheni ya CNN ya Marekani imemfuta kazi mchambuzi wake wa muda mrefu kwa sababu ya kukosoa ukatili na udhalimu wa utawala haramu wa Israel na kutoa wito wa kuundwa nchi huru ya Palestina.

Televisheni ya CNN imechukua hatua hiyo baada ya Marc Lamont Hill kuhutubia kikao cha Umoja wa Mataifa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kuonesha Mshikamano na Taifa la Palestina ambako alitoa wito wa kususiwa Israel na kuundwa nchi huru ya Palestina.

CNN ilitoa taarifa ikisema Marc Lamont Hill amesimamishwa kazi bila kutaja sababu ya ya kuchukuliwa hatua hiyo.

Katika hotuba yake kwenye Umoja wa Mataifa, Mark Lamont Hill ambaye pia ni mhadhiri wa taaluma ya habari katika Chuo Kikuu cha Temple huko Philadelphia alitoa wito wa kususiwa Israel na kuundwa nchi huru ya Palestina  mpaka wake ukianzia 'mtoni hadi baharini' akikusudia kuanzia Mto Jordan hadi Bahari ya Mediterania. Vilevile alisema kuwa anaunga mkono uhuru wa Palestina huku akikosoa vikali sera na mienendo ya Israel.

Baada ya hotuba hiyo makundi ya Kizayuni yanayoiunga mkono Israel nchini Marekani yalianzisha hujuma na mashambulizi makali dhidi ya Mark Lamont Hill na kuitaka televisheni ya CNN na Chuo Kikuu cha Temple kumfuta kazi.

Marc Lamont Hill ametetea hotuba yake hiyo na kusema kauli yake ya 'mtoni hadi baharini' si mwito wa kuangamiza chochote au yeyote. Amesema hotuba yake ilikuwa na wito wa kuwepo haki na uadilifu. Aidha amesisitiza kuwa anaunga mkono uhuru na ukombozi wa Palestina na kwamba ataendelea.

 3467341

captcha