IQNA

Ongezeko la Asilimia 82 la Chuki Dhidi ya Waislamu California, Marekani

22:23 - August 10, 2018
Habari ID: 3471624
TEHRAN (IQNA)- Kumeshuhudiwa ongezeko la asilimia 82 la chuki dhidi ya Waislamu katika jimbo la California nchini Marekani katika mwaka wa 2017 kufuatia kuchaguliwa Donald Trump kama rais.

Hayo yamedokezwa katika ripoti ya  Baraza la Mahusiano ya Kiislamu Marekani (CAIR) ambayo iliorodhesha  malalamikio 2,259 ya matukio ya chuki dhidi ya Waislamu mwaka jana. Aghalabu ya malalamiko yalihusiana na masuala ya ‘usafiri’ au ‘haki za uhamiaji na wahamiaji’ na kwa msingi huo Waislamu walikumbuna na chuki kutokana na amri ya Rais Trump ya kuzuia raia wa nchi zenye Waislamu wengi kuingia Marekani.

Januari mwaka 2017 Trump alitangaza uamusi kuhusu kupiga marufuku watu kutoka Iran, Libya, Somalia, Syria na Yemen kuingia nchini humo. Uamuzi huo wa Trump unaendelea kukosolewa vikali na watetezi wa haki za binadamu kote duniani. “Kutekelezwa marufuku hiyo ya Waislamu kumepelekea Waislamu watazamwe kama tishio kwa usalama wa taifa na hivyo kusababisha kuongezeka ubaguzi unaoungwa mkono na serikali,” imesema sehemu ya ripoti ya CAIR.

Msemaji wa CAIR Marwa Rifahie anasema jimbo la California limeshuhudia ongezeko la chuki dhidi ya Waislamu ambapo mwaka 2015 visa 1,114 viliripotiwa na kuongezeka hadi 1,239 mwaka 2016 na mwaka 2017 kuliripotiwa vitendo  2,259 vya chuki dhidi ya Waislamu, hilo likiwa ni ongezeko la asiliami 82. Kwa ujumla kote Marekani kulishuhudiwa ongezeko la chuki dhidi ya Waislamu na hilo linatokana na sera za kibaguzi za Trump.

Wakati wa kampeni zake, Trump alikuwa ametaka Waislamu wazuiwe kikamilifu kuingia Marekani huku kukiwa na taarifa kuwa, rais huyo wa ameanza kutekeleza mpango wa kuwasajili Waislamu wote Marekani kwa lengo la kudhibiti nyendo zao.

3737292

captcha