IQNA

Waislamu Nigeria watahadharishwa kuhusu athari mbaya za mitandao ya kijamii

8:19 - June 03, 2018
Habari ID: 3471541
TEHRAN (IQNA)- Washindi wa Mashindano ya 15 ya Qur'ani Tukufu ya Lagos nchini Nigeria wametunukiwa zawadi huku Waislamu nchini humo wakitahadahrishwa kuhusu athari mbaya za mitandao ya kijamii.

Washiriki 18 katika kategoria mbali mbali wametunukiwa zawadi Jumapili katika mashindano hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa Chuo Kikuu cha Lagos na kuandaliwa na Jumuiya ya Wanafunzi Waislamu Nchini Nigeria (MSSN) tawi la Lagos.

Washindi wa kategoria ya kuhifadhi Juzuu 15, wanaume, walikuwa ni Bilal Abdur Rasheed (nafasi ya tatu),Muhammad Naeem (nafasi ya pili ) na Umar Muhammad (nafasi ya kwanza). Washindi wa kategoria ya Juzuu 15, wanawake, walikuwa ni  Muminah Bello (nafasi ya tatu), Aabidah Tajudeen (nafasi ya pili ) na Fatimah Adebiaro (nafasi ya kwanza). Halikadhalika kulikuwa na kategoria nyinginezo za kuhifadhi Juzuu 5 na pia Juzuu 3.

Akizungumza katika hafla ya kuwatunuku zawadi washiriki, Ustadh Haroon Thani, Mkurugenzi wa Kituo cha Basmallah cha Kufunza Qur'ani na Uislamu nchini Uingereza alitoa wito kwa serikali ya Nigeria kuwekeza katika ustawi wa vijana. Aidha aliongeza kuwa, "Qur'ani Tukufu si tu ni tumaini la wasio na matumaini bali pia ni tumaini la wenye matumaini. Serikali inapaswa kuwapa matumaini hawa vijana ambao wamejitolea kuhifadhi Qur'ani Tukufu."

Kwa upande wake, Amiri (mwenyekiti) wa MSSN mjini Lagos Dkt. Shaheed Ashafa amewatahadahrisha Waislamu kuhusu athari mbaya za mitandao ya kijamii kwani ni chanzo cha kuvuruga maisha ya kimaanawi ya Waislamu."

Ashafa aliongeza kuwa: "Ni wazi kuwa vijana wengi Waislamu wamejiweka mbali na Qur'ani Tukufu kutokana na athari mbaya za mitandao ya kijamii."

Amesema Waislamu kwa ujumla wamekuwa waraibu wa simu za mkononi, kompyuta n.k na kuzitumia kwa mambo yasiyofaa huku wakijiweka mbali na Qur'ani Tukufu.

Mashindano hayo ya Qur'ani  ambayo nara na kauli mbiu yake ilikuwa ni "Tumaini kwa Wasio na Tumaini" yalifadhiliwa na familia ya marehemu Dkt. Latif Adegbite.

3719287

captcha