IQNA

Kiongozi wa upinzani Uingereza akosoa chuki dhidi ya Uislamu nchini humo

10:44 - February 19, 2018
Habari ID: 3471397
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi wa upinzani Uingereza Jeremy Corbyn ametembelea misikiti kadhaa siku ya Jumapili na kukosoa vikali chuki dhidi ya Uislamu nchini humo.

Kiongozi wa upinzani Uingereza akosoa chuki dhidi ya Uislamu nchini humo

Corbyn ametoa mfano na kusema wanawake Waislamu hubaguliwa na kubughudhiwa katika mitaa ya Uingereza mara kwa mara huku akisisitiza ulazima wa kuwepo maelewano baina ya jamii zote nchini humo.

“Chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) ni tatizo kubwa katika jamii yetu, na ni sawa na aina zingine za ubaguzi… kama ule ubaguzi wanaokabiliana nao watu wenye asili ya Afrika na Caribbean”, amesema Corbyn ambaye pia ni kiongozi cha chama cha Leba alipotembelea Msikiti wa Finsbury Park mjini London.

 

“Nimekuwa na mikitanao na wanawake Waislamu na wamenisimulia visa vya kuogofya kuhusu namna wanavyobaguliwa na kudhalilishwa mara kwa mara katika mitaa yetu. Iwapo mwanamke atadhalilishwa kwa ajili ya kuvaa mtandio, basi atakuwa ametendewa  ovu na hilo ni ovu ambalo sote tumetendewa.”

Msikiti wa Finsbury Park ni kati ya misikiti 200 ambayo siku ya Jumapili ilifungua milango yake kwa wasiokuwa Waislamu ili waweze kujifunza kuhusu Uislamu.

Uchunguzi wa maoni uliofanywa na taasisi ya YouGov na kufadhiliwa na Baraza la Waislamu Uingereza (MCB) unaonyesha kuwa karibu asilimia 70 ya Waingereza hawajawahi kuingia eneo la ibada la itikadi isiyo yao na kwamba asilimia 90 hawajawahi kuingia ndani ya msikiti.

Kufuatia hali hiyo, misikiti 200 kote Uingereza siku ya Jumapili, Februari 18 2018 ilifungua milango kwa ajili ya kuwapokea wasiokuwa Waislamu kwa munasaba wa 'Siku ya Kutumbelea Msikiti Wangu'. Miaka iliyotangulia misikiti kadhaa imekuwa ikiwakaribisha wasiokuwa Waislamu lakini mwaka huu ulishuhudia misikiti mingi zaidi ikishiriki katika mpango huo wa kuwakaribisha majirani ambapo kaulimbiu ya mwaka huu ni 'Milango iliyowazi, misikiti iliyowazi na jamii zilizowazi.'

Wageni wasiokuwa Waislamu waliofika katika misikiti hiyo waliunukiwa zawadi za maua ya waridi, nakala za Qur’ani Tukufu na mitandio.

3465233

 

captcha