IQNA

Mkutano wa Idhaa za Qur'ani Duniani

Idhaa za Qur'ani zikabiliane na ugaidi, misimamo mikali ya kidini

12:27 - February 01, 2018
Habari ID: 3471377
TEHRAN (IQNA)-Mkurugenzi wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kiislamu ya Utangazaji (IBU) Mohamed Salem Walad Boake amesema idhaa za Qur'ani duniani zinaweza kuwa kati ya njia muafaka zaidi za kukabiliana na wimbi la misimamo mikali ya kidini.

Walad Boake ameyasema hayo  Januari 28 katika mkutano wa nne wa idhaa au radio za Qur'ani za ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza kuwa, idhaa za Qur'ani zinaweza kuwa na nafasi muhimu katika kuwaelimisha vijana na kuwazuia kufuata itikadi zenye misimamo mikali ya kidini'

Mkutano huo wa siku tatu uliofanyika mjini Cairo ulijadili kwa kina nafasi ya idhaa za Qur'ani katika kukabiliana na misimamo mikali ya kidini ambayo sasa imekuwa jinamizi katika baadhi jamii za Waislamu duniani.

Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirkiano na Shirika la Kiislamu la Elimu, Sayansi na Utamaduni (ISESCO) pamoja na Jumuiya ya Kitaifa ya Vyombo vya Habari Misri.

Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Waqfu Misri Sheikh Mohammed Mokhtar Goma amesema idhaa za Qur'ani zinaweza kuwa na mchango muhimu katika kukabiliana na misimamo mikali na ugaidi kupitia vipindi vyenye kuelimisha.

Kwa upande mwakilishi wa Chuo Kikuu cha Al Azhar Sheikh Abdul Fattah Awari naye alihutubu katika kikao hicho na kusema misimamo mikali inatokana na tafsiri potovu kuhusu dini. Kwa msingi huo ametoa wito kwa vyombo vya habari vya Kiislamu na taasisi za elimu kuandaa vipindi maalumu vya kuelimisha jamii na kueneza mafundisho sahihi ya Uislamu.

Idhaa za Qur'ani zikabiliane na ugaidi, misimamo mikali ya kidini

Mkutano huo pia ulilenga kuimarisha nafasi na hadhi ya radio  za Qur'ani  duniani na pia kujadili mbinu za kuwavutia vijana katika Uislamu na namna na kukabiliana na wimbi la chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu katika vyombo vya habari vya nchi zisizo za Kiislamu.

Kikao hicho pia kilijadili changamoto za kiufundi katika idhaa za Qur'ani duniani huku washiriki wakijadili njia za kuimarisha uhusiano na kubadilishana vipindi.

3687058

captcha