IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Iran inakabiliana na Wazayuni na Mabeberu wanaozusha vita na mivutano baina ya Waislamu

13:26 - November 24, 2017
Habari ID: 3471277
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imesimama kidete kukabiliana na njama za kambi ya ubeberu na Uzayuni za kutaka kuzusha vita na mivutano baina ya Waislamu na itaendelea kukabiliana na kambi hiyo na kupata ushindi katika mpambano huo kwa idhini ya Mwenyezi Mungu.

Ayatullah Khamenei ameyasema hayo mapema Alhamisi mjini Tehran katika hadhara ya wageni wanaoshiriki katika mkutano wa Wapenzi wa Ahlulbait na Kukabiliana na Matakfiri na kuongeza kuwa, japokuwa kundi la Daesh au ISIS limeangamizwa huko Iraq na Syria lakini hatupaswi kughafilika na hila za maadui, kwa sababu Marekani, Wazayuni na vibaraka wao hawaachi kufanya uadui dhidi ya Uislamu na yumkini wakaanzisha na kutekeleza njama nyingine kama ya Daesh na mfano wake katika eneo jingine.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa Waislamu katika nchi mbalimbali ni hakika inayosimama mbele ya kambi ya ubeberu na ukafiri na kuongeza kuwa: Ulimwengu wa Kiislamu hii leo unaweza kukabiliana na ukafiri na ubeberu, na Mfumo wa Kiislamu nchini Iran ambao uko mbioni kutekeleza kikamilifu sheria za Kiislamu, utakuwa wenzo wa kuwashinda maadui wa Uislamu.

Ameashiria karibu miaka 40 ya njama, mashinikizo na vikwazo vya Marekani na Uzayuni dhidi ya utawala wa Kiislamu nchini Iran na kusema: "Licha ya mashinikizo hayo yote ninatangaza waziwazi kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itatoa msaada mahala popote itakapohitajika kwa ajili ya kupambana na ukafiri na ubeberu na hatutamjali yeyote katika kusema na kuweka wazi jambo hili."Iran inakabiliana na Wazayuni na Mabeberu wanaozusha vita na mivutano baina ya Waislamu

Ayatullah Ali Khamenei amesema kuwa suala la Palestina ndiyo kadhia nambari moja ya ulimwengu wa Kiislamu na kuongeza kuwa, suala la Palestina ndio ufunguo wa kuwashinda maadui wa Uislamu kwa sababu kambi ya ukafiri, ubeberu na Uzayuni ilighusubu nchi ya Kiislamu ya Palestina na kuitumia kama kituo cha kuvuruga amani ya nchi za Mashariki ya Kati; hivyo kuna udharura wa kukabiliana na tezi la saratani la Israel.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, lengo kuu la njama za maadui za kuzusha hitilafu na mifarakano baina ya Waislamu ni kutaka kuudhaminia usalama na amani utawala wa Kizayuni wa Israel. Ameongeza kuwa: Siku Palestina itakaporejeshwa kwa Wapalestina hilo litakuwa pigo kubwa kwa nguzo ya ubeberu, na sisi tutafanya juhudi kwa ajili ya siku hiyo."
3666284
captcha