IQNA

Maulidi ya Mtume SAW nchini Bosnia Herzegovina

13:16 - November 24, 2017
Habari ID: 3471276
TEHRAN (IQNA)-Waislamu nchini Bosnia Herzegovina wanaendelea na sherehe za Maulidi ya Bwana Mtume Muhammad SAW.

Sherehe hizo za Maulidi ambazo zimepewa jina la "Salam ya Rasulallah” zilianza tarehe 20 Novemba katika mji mkuu wa Bosnia Herzegovina, Sarajevo.

Taarifa zinasema idadi kubwa ya Waislamu na watalii mjini humo wanashiriki katika sherehe hizo za kiutamaduni na kidini ambazo zitaendelea kwa siku kadhaa.

Sheikh Farid Davoudovich, mwanachama wa ngazi za juu katika Jumuiya ya Waislamu Sarajevo amesisitiza kuhusu umuhimu wa kusherehekea Maulidi ili kuimarisha mapenzi ya Mtume SAW katika nyoyo za Waislamu.

Aidha ametoa wito kwa Waislamu kufuata Sira ya Mtume SAW katika maisha yao ya kila siku. Maulid ya Mtume SAW itafanyika katika miji yote ya Bosnia Herzegovina hadi Disemba 15 ambapo kutakuwa na maonyesho ya vitabu, mihadhara ya kidini na warsha za kijamii na kiutamaduni.

Kuhusiana na Maulidi au kuzaliwa Bwana Mtume SAW kuna riwaya mbili mashuhuri. Waislamu wengi wa madhehebu ya Kisuni wanaamini kwamba, Bwana Mtume SAW alizaliwa tarehe 12 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka wa tembo uliosadifiana na mwaka 570 Miladia. Kundi jengine la Waislamu ambalo linaundwa zaidi na Waislamu wa madhehebu ya Kishia linaamini kwamba, Mtume wa Uislamu alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiul Awwal mwaka huo huo.

3665452
captcha