IQNA

Waislamu 50 wauawa katika hujuma ya kigaidi msikitini nchini Nigeria

23:43 - November 21, 2017
Habari ID: 3471273
TEHRAN (IQNA)- Waislamu wasiopungua 50 wameuawa katika hujuma ya kigaidi dhidi ya msikiti mmoja ulioko kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Waislamu 50 wauawa katika hujuma ya kigaidi msikitini nchini NigeriaMsemaji wa Polisi katika jimbo la Adamawa, Othman Abubakar watu hao wamepoteza maisha kufuatia mripuko wa bomu uliotokea mapema leo Jumanne katika mji wa Mubi, wakati Waislamu walipokuwa wakiingia msikitini hapo kwa ajili ya Sala ya alfajiri.

Amesema kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram ndilo limehusika na shambulizi hilo, na kwamba idadi ya watu waliojeruhiwa ni kubwa mno ingawaje hawana takwimu rasmi kwa sasa.

Naye Bayi Muhammad, mmoja wa waumini wanaokwenda katika msikiti huo na ambaye ameshuhudia tukio hilo amesema baadhi ya wahanga wa hujuma hiyo ya kikatili wameteketea kiasi cha kutotambulika.

Shambulizi hilo la kigaidi linahesabiwa kuwa mauaji makubwa zaidi ya umati nchini Nigeria mwaka huu.

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya magaidi wanne wa Boko Haram kujiripua kwa bomu mjini Maiduguri, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo ambapo mbali na watu 18 kuuawa, wengine 30 walijeruhiwa.

Kundi la Boko Haram lilianzisha mashambulizi yake ya kigaidi mwaka 2009 ambapo hadi sasa zaidi ya watu elfu 20 wameuawa nchini Nigeria, Cameroon, Chad na Niger.

Neno Boko Haram kwa lugha ya Kinigeria ya Kihausa lina maana ya 'elimu kutoka nchi za Magharibi ni haramu'. Kundi hilo la Boko Haram ambalo lina ufahamu usio sahihi na potovu kuhusu dini ya Kiislamu, limekuwa likitekeleza hujuma katika maeneo mbalimbali ya Nigeria hasa kaskazini mwa nchi hiyo.

3665551

captcha