IQNA

Qarii kutoka Kenya apongeza mashindano ya Qur'ani nchini Iran

16:02 - December 24, 2016
Habari ID: 3470757
IQNA-Qarii (msomaji) wa Qur'ani Tukufu kutoka Kenya amesema Mashidano ya 6 ya Kimataifa ya Qur’ani ya Wanachuo Waislamu yatakayofanyika nchini Iran ni fursa ya kujimmarisha katika ujuzi wa Qur'ani.

Katika mahojiano na IQNA, Qarii Salim Mohammad Salim ambaye atawakilisha Kenya katika mashindano hayo amesema yatakuwa jukwaa la kujifunza kuhusu harakati za Qur'ani katika nchi zingine duniani na mbinu zinazotumika kufundisha usomaji wa Qur'ani.

Aidha amesema mashindano hayo ya Qur'ani yatakuwa fursa ya kuwahimiza vijana kujifunza Zaidi Qur'ani na kuhifadhi aya zake.

Mashindano ya 6 Kimataifa ya Qur’ani ya Wanachuo Waislamu yamepangwa kufanyika Januari 31 hadi Februari 3 2017 katika mji mtakatifu wa Mashhad, kaskazini mashariki mwa Iran.

Akademia ya Elimu, Utamaduni na Utafiti Iran (ACECR) imekuwa ikiandaa mashindano hayo ya Qur’ani maalumu kwa wanafunzi Waislamu wa vyuo vikuu tokea mwaka 2006 kwa lengo la kuimarisha umoja wa Kiislamu na kuleta ushirikiano miongoni mwa wanafunzi Waislamu sambamba na kuinua kiwango cha harakati za Qur'ani.

Qarii Salim amesema alihudhuria mashindano yaliyopita na ana matumaini kuwa mara hii atafanikiwa kushinda zawadi.

Aidha qarii huyo kutoka Kenya amesistiza kuhusu umuhimu wa kutekeleza mafundisho ya Qur'ani sambamba na kusoma na kuhifadhi kitabu hicho kitukufu.

Akiashiria kuhusu harakati zake za Qur'ani, Salim anasema alianza kujifunza qiraa na hifdhi ya Qur'ani akiwa na umri wa miaka 5 na angali anaendeleza harakati hiyo.

Qarii Salim, ambaye anaishi katika mji wa Mombasa katika pwani ya Kenya, anasema ingawa waliowengi nchini humo ni Wakristo lakini kuna madrassah na vituo vingi vya kufundisha Qur'ani Tukufu nchini humo.

3555542

captcha